Wafanyabiashara wa Tanzania wamesema wapo tayari kwa kufanya ushirikiano wa kibiashara wa ubia na wafanyabiashara kutoka nje ili kukuza diplomasia ya kiuchumi na mataifa mengine.
Akizungumza katika hafla ya chakula cha mchana na mabalozi wa Tanzania nje ya nchi kilichoandaliwa na Taasisi ya sekta binafsi (TPSF) nchini, Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Dkt. Reginald Mengi amesema wafanyabiashara watanzania si omba omba na wapo tayari kwa kufanya biashara ya ubia na wenzao.
“Napenda kusisitiza kwamba sisi watanzania si omba omba kwa wafanyabishara wa nje, tuna nia uwezo, ujuzi na tunajiamini kwa kufanya biashara za kimataifa kwa ubia ili kukuza uchumi wa nchini zetu,” amesema Dkt. Mengi.
Amesema kwamba fursa za uwekezaji zipo nchini kwenye sekta za kilimo, mafuta, gesi, usindikaji na mawasiliano ila ni muhimu kuunganisha nguvu za wafanyabiashara ili kuweza kupata matokeo chanya.
Dkt. Mengi alilisisitiza kwamba sekta binafsi nchini ina imani kubwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli katika adhma yake ya kukuza sekta ya viwanda ili kutatua tatizo la ajira na kuongeza mapato ya nchini.
“Ni muhimu kuimarisha sekta binafsi ili iweze kutoa mchango mkubwa katika uanzishwaji wa viwanda hapa nchini, kwa vyovyote vile sekta hii binafsi ndio itakayojenga viwanda hapa Tanzania,” aliongeza
Kwa Upande wa Mabalozi, Dkt. Emmanuel Nchimbi ambaye anakwenda kuiwakilisha nchi huko Brazil, amesema kwamba mabalozi ni kiungo muhimu kati ya wananchi wa mataifa husika katika kukuza mahusiano na ushirikiano wa kimataifa.
“Sisi ni wawakilishi wenu huko kwenye mataifa ya nje na zaidi na kukuza mahusiano au diplomasia ya kiuchumi kwa maslahi ya wananchi wetu,” amesema Dkt. Nchimbi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye akiwasilisha 'presentation' iliyoainisha maeneo muhimu ya fursa za kibiashara kwenye masoko ya kimataifa kwa mabalozi wapya wa Tanzania nje ya nchi walioapishwa hivi karibuni wakati wa hafla ya chakula cha mchana kwa mabalozi hao iliyoandaliwa na TPSF jijini Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Dkt. Reginald Mengi akisisitiza jambo kwa mabalozi wapya watakaoiwakilisha Tanzania kwenye nchi za Uturuki, Italy, China, Brazil na UN Geneva (hawapo pichani) katika hafla ya chakula cha mchana na kuwapongeza mabalozi hao iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini–CTI Dr. Samwel Nyantahe akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika uwekezaji, kutafuta masoko mapya, kubadilishana bidhaa na utafutaji fursa za biashara kwenye masoko ya kimataifa kwa wafanyabiashara katika hafla ya chakula cha mchana na kuwapongeza mabalozi wapya watakaoiwakilisha Tanzania kwenye nchi za Uturuki, Italy, China, Brazil na UN Geneva iliyoandaliwa na TPSF katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam
Balozi mpya wa Tanzania nchini Uturuki, Prof Elizabeth Kiondo akitoa shukrani kwa TPSF kwa kuandaa hafla fupi kama hiyo ya kubadilishana mawazo kwa jinsi gani wanaweza kukuza diplomasia ya kiuchumi katika vituo vyao vya kazi walipopangiwa.
Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki, akizungumza kwenye hafla hiyo ambapo amesisitiza wafanyabiashara kutoka Tanzania watumie fursa adimu ambayo ipo kati ya Tanzania na China ambapo mahusiano na ushirikiano ulianza tangu enzi za Mao na Mwalimu Nyerere.
Balozi wa Tanzania, Geneva, Dkt. James Msekela akisisitiza jambo kwa bodi ya TPSF kwenye hafla ya chakula cha mchana kwa mabalozi hao wapya iliyofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
HABARI ZAIDI BOFYA HAPA