Na Chalila Kibuda, Globu ya Jamii.
Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kipindi cha Julai mpaka Desemba 2016 zilifanya ukaguzi katika baadhi ya migodi mikubwa nchini na kampuni za uchimbaji madini kulipa kodi na kufanikiwa kukusanya Sh. bilioni 79.26
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Habari TMAA, Mhandisi Yisambi Shiwa, amesema fedha zilizopatikana zililipwa serikalini ikiwa ni kodi ya mapato iliyotokana na ukaguzi huo. Amesema katika ukaguzi huo Kampuni ya Geita Gold Mining Limited imelipa Sh. biliioni 45.76 pamoja na Kampuni ya North Mara Limited imelipa sh. bilioni 33.5
Mhandisi Yisambi amesema ukaguzi wa madini ya ujenzi na viwandani uliofanywa na wakala kwa kushirikiana na Ofisi za Madini Kanda za Kaskazini,Mashariki,Kusini pamoja na Magharibi umesaidia kuongezeka kwa malipo ya mrabaha serikalini kwa kiasi cha sh. bilioni 3.8.
‘’Kiasi cha mrabaha huo kimetokana na uzalishaji wa tani milioni 6.8 za madini ya ujenzi na viwandani yenye thamani ya shilingi bilioni 119.5’’amesema Shiwa.
Aidha amesema kupitia madawati ya ukaguzi yaliyopo katika Viwanja vya Ndege Nchini Wakala kwa kushirikiana na taasisi za serikali wamekuwa wakiwakamata watu wanaosafarisha madini nje ya nchi kinyume cha sheria walipigwa faini ya Dola za Kimarekani 91,924.38 katika kipindi cha Julai na Desemba 2016.
‘’Wahusika waliohusika na sakata la usafirishaji wa madini nje ya nchi walichukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010.
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha habari TMAA, Mhandisi Yisambi Shiwa Akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu shughuli mbalilmbali zinazowafanywa na wakala wa ukaguzi wa madini leo jijini Dar es Salaam. Kulia Kaimu Mkurugenzi Uzalishaji na Biashara ya Madini , Migodi ya Kati na Midogo, Mhandisi George Manyama. Picha na Emmanuel Massaka,Globu ya Jamii.