Na Greyson Mwase, Dar es Salaam.
Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar zinatarajia kuunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuandaa Mpango wa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika sekta za gesi na mafuta.
Hayo yalielezwa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo katika kikao chake na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib aliyeambatana na Ujumbe wake.
Wengine waliohudhuria kikao hicho ni watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA) na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA).
Profesa Muhongo alisema lengo la kamati hiyo ni kujadili maeneo ya kushirikiana pamoja na kubadilishana uzoefu katika sekta za gesi na mafuta
Alisema kuwa, kamati hiyo itashirikisha Wataalam kutoka katika taasisi za Sheria, Ardhi, Kodi, Gesi na Mafuta chini ya Makatibu Wakuu wa sekta husika kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.Waziri Muhongo alisema kuwa, uwepo wa kamati hiyo utachochea Zanzibar kuwa na taasisi kama TPDC na nyingine hivyo kupelekea ukuaji wa sekta ya gesi na mafuta.
Alisisitiza kuwa, Serikali ya Tanzania Bara kupitia Wizara ya Nishati na Madini ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Zanzibar pamoja na kubadilishana uzoefu katika masuala ya gesi na mafuta.Profesa Muhongo alishauri Serikali ya Zanzibar kuandaa wataalam wa mafuta na gesi kwa kuwasomesha katika ngazi za diploma na shahada katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Madini Dodoma (MRI).
Akiongeza kuwa, Serikali ipo tayari kutoa ufadhili kwa wanafunzi wa Zanzibar wanaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kwa ajili ya kusomea shahada ya uzamili katika vyuo vya ndani na nje ya nchi.Naye Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib, alimshukuru Waziri Muhongo kwa utayari wa Wizara ya Nishati na Madini katika kushirikiana na Wizara yake kwenye shughuli za mafuta na gesi
Alisema kuwa, kamati itakayoundwa itapelekea mambo kwenda kwa kasi na kuwa na data za pamoja zinazotokana na utafiti wa mafuta na gesi na kupanga Mikakati ya kuvutia wawekezaji kutoka nje ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Msomba ( wa tano kushoto, waliokaa mbele) akielezea majukumu ya shirika hilo katika kikao cha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib aliyeambatana pamoja na ujumbe.
Mkurugenzi wa Mkondo wa Chini wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dk Wellington Hudson akieleza jambo katika kikao hicho.
Kaimu Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Venosa Ngowi akielezea shughuli za utafiti zinavyofanyika katika shirika hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Venosa Ngowi akielezea shughuli za utafiti zinavyofanyika katika shirika hilo.
Kaimu Mkurugenzi wa Mkondo wa Juu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Venosa Ngowi akielezea shughuli za utafiti zinavyofanyika katika shirika hilo.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati, waliokaa mbele) na Waziri wa Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira Zanzibar, Salama Aboud Talib ( wa pili kutoka kushoto, waliokaa mbele wakiwa katika picha ya pamoja na watendaji kutoka Wizara husika.