Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
KUFUATIA kuzuka kwa tetesi zinazodai kocha wa timu ya Azam FC Zeben Hernandez kutokubali kiwango cha shambuliaji wa timu hiyo John Bocco, uongozi wa timu hiyo ubeibuka na kudai kuwa mwalimu huyo bado hajatoa tathmini yake.
Uongozi huo kupitia kwa Katibu Mkuu wake Saadi Kawemba umasema kuwa kocha huyo anatarajiwa kutoa tathmini ya timu hiyo toka alipoanza kuifunzisha rasmi Jumatatu ya wiki ijayo na anashangazwa na taarifa hizo kwani kama wao kama uongozi hawajapokea taarifa zozote kutoka kwa mwalimu inakuaje watu wa nje wanaongea kitu wasichokijua.
Azam iliingia kambini mwanzoni mwa mwezi huu kwa ajili ya kujiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ikiwemo kucheza mchezo mmoja wa kirafiki kama majaribio kwa wachezaji wao waliokuja katika majaribio.
Baada ya kuanza na ushindi wa goli 2-0 dhidi ya Ashanti united sasa timu ya Azam FC inatupa karata yake nyingine leo kwa timu ya Friends Rangers.
Mchezo huo utakuwa wa pili wa kifariki kwa ajili ya kuwapima wachezaji wao wapya waliopo kwenye majaribio kabla ya kuanza rasmi kwa mechi zao za kifariki.
Kuelekea msimu ujao timu hiyo imepanga kuwa na kikosi bora zaidi ili kutimiza adhma yao ya kunyakua ubingwa baada ya Yanga kutwaa taji hilo misimu miwili mfululizo. Afisa habari wa timu hiyo Jaffar Idd Maganga amesema kuwa baada ya kucheza na kupata ushindi dhidi ya Ashanti sasa wanawageukia Friends Rangers na michezo hiyo itaendelea kupima uwezo wa wachezaji wao wapya ambao wamekuja ndani ya Azam kwa ajili ya majaribio.
Amesema kuwa wameamua kufanya hivyo kutokana na wachezaji hao uja kwa nyakati tofauti hivyo wale watakaofuzu majaribio watakuwa nao katika michezo mingine hasa ya kirafiki ya kimataifa, "Mwalimu aliomba mechi za kirafiki za mapema ili kuangalia uwezo wa wachezaji waliokuja katika majaribio huku tukiamua timu yetu icheze na timu za daraja la kwanza kwani zimekuwa kambini kutokana na kushiriki mashindano mbalimbali pia ni nzuri kwani zimekuwa zikitupa wakati mgumu."