NA MWANDISHI WETU, DODOMA
BENKI ya CRDB imetoa msaada wa vifaa vya michezo kwa wabunge wa Jamhuri la Muungano wa Tanzania.
Vifaa hivyo vilikabidhiwa na Mkurugenzi wa benki ya CRDB Tawi la Dodoma, Rehema Hamis na kupokelewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Vifaa vilivyokabidhiwa ni jezi seti mbili ikiwamo ya golikipa, viatu, mpira, soksi na suti za michezo ambavyo vimegharimu zaidi ya Sh. Milioni 5.
Awali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, aliwapongeza wafadhili na wadhamini wanaojitokeza kusaidia sekta ya michezo na kuwataka wengine waige mfano huo, kwani hivi sasa michezo ni uchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi kutoka makao makuu ya CRDB anayeshughulikia Mikakati na Ubunifu, Goodluck Nkini, alisema wameamua kutoa vifaa hivyo kutokana na mapenzi yao kwa wananchi hususan wateja wao, ambao wabunge ndio wawakilishi wao.
“Pia ni katika mpango wa taasisi kuunga mkono katika kazi, kwani michezo mbali ya burudani hujenga afya, hivyo wabunge na wafanyakazi wa CRDB wakiwa na afya njema watatekeleza vema majukumu yao,” alisema Nkini.
Jioni ulipigwa mchezo wa kirafiki kati ya Bunge FC na CRDB kwenye Uwanja wa Jamhuri na kumalizika sare ya bao 1-1.
Walikuwa ni CRDB walioanza kuzifumania nyavu za Bunge FC dakika ya 49 mfungaji akiwa Faisal Mbuya.
Bunge FC walicharuka na kuwachukua dakika sita tu kuchomoa dakika ya 55 kwa bao la Yusuf Gogo. Hadi mwamuzi Peter Mdachi akipuliza kipenga kuashiria dakika 90 kumalizika, hakuna aliyeibuka mbabe.
Mkurugenzi wa Benki ya CRDB tawi la Dodoma, Rehema Hamis akizungumza kabla ya kukabidhi vifaa vya michezo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (kulia) akipokea msaada wa vifaa vya michezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Benki ya CRDB tawi la Dodoma, Rehema Hamis kwa ajili ya timu ya soka ya Bunge. Makabidhiano hayo yalifanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma mwishoni mwa wiki. Wa pili kulia ni Naibu Spika Dk. Tulia Akson, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa na kushoto ni Mkurugenzi wa Mikakati na Ubunifu wa Benki ya CRDB, Goodluck Nkini.